Home Makala Shaka Zulu: Baba wa taifa la Zulu

Shaka Zulu: Baba wa taifa la Zulu

Jina la Shaka Zulu mara nyingi linaambatanishwa na vita. Jeshi lake liliteketeza kila aliyetaka kulipinga. DW imezungumza na mwanahistoria Maxwell Shamase anaesema urithi wa Shaka umetafsiriwa sivyo.

    

Shaka Zulu: Baba wa taifa la Zulu

Mengi yamesemwa kuhusu Shaka Zulu. Lakini Dokta Maxwell Zakhele Shamase ana uwezo mzuri wa kutenganisha ukweli na uongo. Akishirikiana na Mthandeni Patrick Mbatha, mwanahistoria kutoka Chuo Kikuu cha Zululand ameamua kuandika kitabu kuhusu maisha ya Shaka Zulu.

DW: Kwanini umeamua kuandika kitabu kuhusu Shaka Zulu?

Maxwell Shamase: Kuna machache tu yaliyoandikwa kuhusu maisha ya Mfalme Shaka Zulu kwa mtazamo wa Kiafrika. Baadhi ya mambo yanayoandikwa na watu wasio Waafrika kwa hakika hayana ukweli. Tunataka kuhadithia maisha yake kwa mtazamo wa Kiafrika.

Vipi unaweza kumuelezea Shaka Zulu?

Kabla ya kuzaliwa kwa Shaka, nabii kwa jina la Sithayi, alibashiri kwamba ‘kutazaliwa mtoto ambaye ataleta mfumo mpya wa utawala na kuanzisha taifa jipya.’ Alikuwa ni mjuzi wa mikakati ya vita barani Afrika. Alikuwa ni mjenzi wa taifa na sio kiongozi anaependa kumwaga damu. Hakuwa muuwaji asiye na huruma.

Shaka Zulu: Baba wa taifa la Zulu

Shaka alizaliwa lini na wapi?

Alizaliwa 1787 miongoni mwa watu wa kabila la eLangeni alikotokea mama yake.

Jina la Shaka Zulu limetokea wapi?

Baba yake akiitwa Senzangakhona na mama yake alikuwa ni bintimfalme Nandi kutoka familia ya kifalme ya Mhlongo aliyeishi katika eneo la eLangeni. Jina Shaka linatokana na ugonjwa unaoitwa “ishaka”. Ugonjwa huu ulikuwa ukiwafanya wanawake wasikie maumivu, wanakuwa wavivu, na miili yao kufura. Wakati mama yake aliposhika mimba yake nje ya ndoa, watu kwanza walidhani naye amekumbwa na ugonjwa wa ishaka. Na hivyo ndivyo Shaka alivyolipata jina lake la Shaka Senzangakhona.

Miaka hiyo, jina la ukoo linatoka upande wa baba. Na babu yake Shaka akiitwa Zulu. Alipokuwa mfalme, Shaka alisema hebu tuwe na utambulisho na tujiite watu wa Zulu. Alikuwa ni mtu wa kwanza kuwapa watu wake jina la “Zulu” na wakawa watu wa Zulu. Na hadi hii leo anajulikana kama mwanzilishi wa taifa la Zulu licha ya kwamba alirithi kiti cha enzi cha ufalme ulioachwa na vizazi vilivyopita.

Je, Senzangakhona, alimkubali kuwa ni mtoto wake? 

Kwanza alijaribu kumkana kama sio mtoto wake kwa sababu alikuwa akimuogopa sana baba yake,  Mfalme Zulu. Ni kitendo cha aibu kubwa kwa mwanamflame kumpa mimba msichana nje ya ndoa ambacho adhabu yake inaweza kumkosesha kiti cha ufalme. Baadae alimkubali kuwa ni mtoto wake, na akalipa mahari na Nandi akahamia kwenye familia ya Senzangakhona.

Nandi and Shaka  walifukuzwa baadae katika familia ya Senzangakhona. Ilikuaje?

Nandi alikuwa ni mtu mwenye kiburi na alipenda kuamrisha watu. Kwahiyo uhusiano wao ulikuwa na misukosuko. Senzangakhona hakuweza tena kumvumilia. Alimfukuza pamoja na mtoto wake Shaka. Baadae Nandi alikutana na Ngwati. Walipendana na pamoja walizaa mtoto wa kike.

 African Roots + Shaka ZuluAsili ya Afrika/Shaka Zulu

Ngwati aliuawa. Nandi na watoto wake wawili walichukuliwa na mfalme wa Mthethwa, Dingiswayo. Vipi Shaka alijiunga na jeshi la Mthethwa?

Alikuwa msaidizi wa Mfalme Dingiswayo wakati akiwa na umri wa miaka 16. Alipata nafasi hiyo kutokana na uwezo wake na ujasiri aliokuwa nao. Muda mfupi baadae alichaguliwa kujiunga na jeshi la Izicwe.

Shaka Zulu alikuwa na ushawishi gani katika jeshi la Mthethwa?

Kama kamanda, waliwalazimisha mashujaa wake kutovaa viatu na kutembea pekupeku. Alizuia pia matumizi ya mikuki mirefu ambayo mashujaa wake waliitumia dhidi ya maadui wao. Badala yake aliwataka watumie mikuki mifupi ‘Iklwa’ kwa mapambano ya karibu zaidi. Mkakati huu uliwalazimisha wapiganaji wake kutumia mkuki mmoja kupigana na maadui wengi zaidi. Alianzisha pia mkakati wa kuwazunguka wapinzani wao kabla ya kuwavamia, maarufu kama “pembe za nyati.” Shaka Zulu alikuja kuwa mtu anaeogopwa sana na kupata umaarufu hata kwenye makabila na falme nyinginezo, hadi akapewa jina la ‘Nodumehleli’ linalomaanisha yule ambaye akiketi ardhi kutikisika.

Alipata ufalme wa Senzangakhona wakati bado akiwa mpiganaji wa jeshi la Mthethwa. Je, kitendo hiki kiliangaliwa vipi?

Baba yake Senzangakhona alipofariki, Mfalme Dingiswayo alimsaidia kurudi kwa watu wa baba yake, na kumpa mashujaa wawili kuongozana naye kumsaidia kukamata madaraka. Lakini Mfalme Senzangakhona alimwambia waziri mkuu wake Mudli, kwamba mtoto mwengine wa kiume Sigujana ndiye atakaerithi kiti cha ufalme, na sio Shaka. Alipowasili, Shaka alimuuwa Sigujana na mwaka 1816 alijitangaza Mfalme. Baada ya Mfalme Dingiswayo kufariki, Shaka aliwajumuisha watu wa Mthethwa chini ya ufalme wake.

Shaka hakutaka kuoa na kuna waliodai pengine alikuwa shoga. Kwanini hakuunga mkono suala la ndoa?

Shaka hakuunga mkono suala la ndoa kutokana na alivyoshuhudia yaliyomkuta mama yake. Na utotoni mwake mara nyingi alikuwa akifanyiwa utani kwa vile hakulelewa na baba yake. Alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanawake tofauti, lakini pindi wakishika mimba alikuwa alimtunukia ndugu yake wa kiume ambaye alikuwa akionekana kama mtu dhaifu.

 African Roots + Shaka ZuluAsili ya Afrika/Shaka Zulu

Je, kweli Shaka Zulu aliwaua wanawake aliowapa mimba, kama inavyodaiwa?

Madai hayo hayawezi kuwa kweli. Kuna simulizi moja inayoeleza jinsi wafanyabiashara wa kizungu walivyomfufua mwanamke aliyeanguka kutoka na homa kali. Shaka alitaka kujua hakika kama kweli wafanyabiashara hao wa kizungu wana uwezo wa kufufua binadamu. Aliamrisha mwanamke mmoja auliwe, na kuwataka wazungu hao wamfufue kitu kilishowashinda bilashaka. Kuna wakati, kwa sababtu ya udadisi, inasemekana Shaka alichana tumbo la mwanamke mjamzito ili kujionea jinsi mtoto anavyokuwa ndani ya tumbo la mama yake.

Tunaambiwa Shaka aliua watu wapatao milioni moja, baadhi yao bila ya makossa yoyote isipokuwa kwa vile walikuwa na kimo kifupi. Je hayo ni maneno ya kweli?

Huo ni mtazamo wa Kimagharibi na sio jambo lilotokea kweli. Kumbuka kwamba, watu milioni 50  waliuawa katika vita vya pili vya dunia pamoja na mamilioni wengine waliouawa wakati wa vita vya kwanza vya dunia. Je, nani mbaya Zaidi kati ya Shaka na wazungu waliopigana vita vya kwanza na vya pili vya dunia? Aidha, mauaji ya aina hiyo yalikuwa yakikubalika nyakati hizo. Kwa mfano, wachawi waliuliwa. Mfalme alinusurika kwa kuwaua wapinzani wake.

Kifo cha Zulu kilikuaje?

Aliuliwa mnamo mwaka 1828. Kulikuwa na njama iliyopangwa na shangazi yake. Sababu kuu ni kwamba baada ya kifo cha mama yake Shaka alirukwa na akili na akawa anaua watu bila ya kufikiria mara mbili kwa kisingizio cha kuwa na huzuni ya kufiwa na mzazi wake. Baadhi aliwaua kwa kumfanyia utani utotoni mwake, na wengine aliwaua kwa kutoonyesha huzuni vya kutosha wakati wa kifo cha mama yake.

Asili ya Afrika/Shaka Zulu

Je, kuna ubaya wowote wa kumfananisha Shaka na Napoleon na kumwita Napoleon mweusi?

Alikuwa ni mbabe wa kivita na sio Napoleon mweusi. Kwanini usiseme Napoleon alikuwa Shaka mweupe? Hakuwahi kwenda Ulaya, na hakuna mzungu aliyemfunza mikakati aliyoitumia wakati wa vita. Yote ilikuwa ni mipango yake mwenyewe.

Je, Shaka Zulu ana mchango wowote miaka ya leo?

Shaka ni gundi inayowaunganisha watu wa Zulu. Chama cha Inkatha Freedom kinachoongoza katika jimbo la Kwazulu Natal linamtambua Mfalme Shaka. Wafalme wa Zulu pamoja na watu wao bado wanamuenzi Mfalme Zulu hadi hii leo.

Mtaalam wa historia ya Zulu, Maxwell Zakhele Shamase, mwenye shahada ya uzamivu PhD ya somo la Historia – Siasa za Kisasa na historia ya Wazulu, historia ya mkoa wa watu wa jimbo la Kwazulu Natal. Hivi sasa anaandika kitabu juu ya Mfalme Shaka. Shamase pia ni mhadhiri na Mkuu wa Idara ya Historia katika Chuo Kikuu cha Zululand kinachojulikana pia kama Chuo Kikuu cha Unizulu.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.

(Visited 4 times, 1 visits today)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here