Home Mahusiano Vidokezo 8 vya usafi kwa wanaume na wanawake kabla na baada ya...

Vidokezo 8 vya usafi kwa wanaume na wanawake kabla na baada ya kujamiiana

Kunawa mikono ni jambo muhimu zaidi siku hizi kuliko ilivyokuwa zamani, lakini je watu wananawa mikono kabla na baada ya kufanya tendo la ndoa?

Hili ni swali ambalo huenda la kudhalilisha- kwa mfano kabla ya tendo la ndoa ukimuuliza mpezi wako “umenawa mikono?” – lakini wataalamu wa masuala ya kujamiiana wanasisitiza umuhimu wa kuzingatia usafi katika uhusiano wa kimapenzi.

Ni hatua muhimu ambayo inaweza kukuepusha kwa mfano na magonjwa yanayoathiri sehemu za siri.

“Kunawa mikono na kusafisha meno ni muhimu kwasababu viungo hivyo vinatumika sana wakati wa tendo la ndoa,” Thamara Martínez Farinós, mwanasaikolojia na mtaalamu wa masuala ya ngono kutoka Taasisi ya Espill Institute, mjini Valencia, Uhispania ameiambia BBC Mundo.

Kando na kunawa mikono pia ni muhimu kuosha sehemu za siri kila siku. Lakini “kuosha haraka haraka” haitoshi, alifafanua mtaalamu huyo.

“Usafi ni muhimu kwa sababu unasaidia kuzuia magonjwa ya zinaa yanayoambukizwa kupitia ngono”, Vicente Briet, mwanasaikolojia na mtaalamu wa saikolojia ya kujamiiana, ameiambia BBC Mundo.

Mkurugenzi wa kituo cha matibabu cha Vicente Briet na mkuu wa kitengo cha saikolojia ya ngono katika Chuo Kikuu cha Alicante nchi Uhispania anasema usafi “ni chanzo kikuu cha hamasa wakati wa tendo landoa”.

Na kuongeza kuwa “Ukuzaji wake unaanza na umuhimu tunaopatia usafi wa miili yetu kabla na baada ya kushiriki tendo la ndoa .”

Usafi huu unaweza kuzingatiwa vipi.

Kwa wanaume…

Mtandao wa Huduma ya Afya ya Umma ya Uingereza (NHS) unaelezea jinsi wanaume na wanawake wanavyotakiwa kusafisha maeneo yao ya siri.

Madaktari wanapendekeza wanaume kuosha sehemu zao kwa kutumia maji ya uvuguvugu kila siku kwa kuangazia zaidi maeneo ambayo huenda yakachangia kukusanyika kwa bakteria, kwa kutumia sabuni ambayo inakabiliana na viini vinavyosababisha bakteria

“Suluhisho la kukabiliana na bakteria wanaoshambulia maeneo ya siri kwa wanaume ni kuzingatia usafi wa mara kwa mara,”anasema Dk. Briet.

Je unazingatia usafi wakati wa tendo la ndoa?
Maelezo ya picha,Je unazingatia usafi wakati wa tendo la ndoa?

“Inashangaza jinsi baadhi ya wanaume wanavyopuuza usafi wa kimwili hususani katika sehemu zao za siri. Sio tu kwamba hali hiyo huleta matatizo yanayotokana na usafi duni, lakini pia ni changamoto kwa wenzi wao, ” aliandika Patrick French, mtaalamu wa afya ya uzazi katika mtandao wa NHS .

“Iwe ni kutokana na kutojua, baadhi ya wanaume wanafanya kosa la kutosafisha maeneo yao ya siri, licha ya athari za kiafya ambazo huenda zikatokana na hatua hiyo kama vile: harufu mbaya na maambukizi ya magonjwa,” aliamibia BBC Mundo.

NHS hata hivyo inaonya wanaume kutotumia sabuni wakati wanaposafisha sehemu za siri kwani maji ya vuguvugu yanatosha kuua viini.

Na ikiwa lazima watumie sabuni wataalamu wanapendekeza itumike kwa “kiwango kidogo tena isiwe na marashi ili kuzuia muwasho wa ngozi.”

Kwa wanawake…

Wataalamu wa afya ya uzazi wanakubaliana kwamba kuna upotoshaji mwingi unaoshuhudiwa, licha ya kwamba kuna kampuni nyingi zinazojihusisha na “usafi wa sehemu za siri” za wanawake

Kujiosha kwa makini sehemu za siri ni muhimu, lakini sio lazima utumie sabuni yenye manukato.

“Uke umeumbwa kwa njia ambayo inajisafisha yenyewe kiasilia. Lakini hiyo haimaanishi sehemu hiyo haihitaji kuoshwa, ” Taarifa ya mtandao wa NHS inasema.

“Kuna aina nyini ya bakteria ndani ya uke ambayo ipo hapo kama kinga,” aliongeza mtaalamu Thamara Martínez..

Wataalamu wa saikolojia ya kujamiiana wanatahadharisha matumizi ya sabuni yenye manukato kusafisha uke kwasababu haihitajiki na pia ni hatari.

“Sehemu ya nje ya uke inaweza kusafishwa kwa sabuni isiyo na manukato ama bidhaa maalum zilizotengenezwa kwa ajili ya kusafisha sehemu hiyo”, anasema Thamara Martínez.

“Pia inategemea ngozi ya mtu, kuna nyingine huenda zikasababisha muwasho ambao unaongeza hatari ya kupata magonjwa. Kile ninachopendekezwa ni kusafisha sehemu za siri angalau mara moja kwa siku.”

Uke umeumbwa kwa njia ambayo inajisafisha wenyewe kiasilia.

Baadhi ya athari za kiafya zinazosababishwa na utumiaji wa sabuni yenye manukato kuosha uke ni pamoja na :

 • Kubadilika kwa hali ya kawaida ya mazingira asilia ya sehemu za siri kwa wanawake
 • Kuwashwa
 • Kukauka kwa hali ya unyevu (ambako kunasaidia uke kudumisha mazingira yake ya kawaida)
 • athari ya mzio
 • kuongeza hatari ya kupata maambukizi

Wanaume na wanawake

Kidokezo kimoja ambacho kinastahili kuzingatiwa na jinsia zote mbili kwa mujibu wa wataalamu ni kwamba wanaume na wanawake wanashauriwa kwenda haja ndogo kabla na baada ya kufanya tendo la ndoa.

“Kwenda haja ndogo baada ya kufanya tendo la ndoa ni moja ya njia muhimu ya kujiepusha na magonjwa yanayosababishwa na bakteria, ” anasema Martínez.

“Kujisaidia haja ndogo baada ya tendo la ndoa kunasaidia kusafisha kibofu cha mkojo, hali ambayo inazuia bakteria kuathiri sehemu hiyo,” anaeleza

“Pia kwenda haja ndogo kabla ya tendo la ndoa ni muhimu, kwani wapenzi watakaribiana bila kuwa na hofu .”

Briet anaongeza kuwa mwenendo huo “ni mzuri kwani unaweza kuzuia magonjwa yanayoathiri njia ya kupitisha mkojo kwa kiwango kikubwa hata kama sio magonjwa mengine.”

Wataalamu wa saikolojia ya ngono wanapendekeza wapenzi kwenda haja ndogo “punde baada ya kufanya tendo la ndoa” ili kujikinga na magonjwa na kupunguza uwezekano wa kuambukizwa magonjwa.

Kulingana na wataalamu hao wanawake wako katika hatari ya kupata maabukizi ya magonjwa yanayoathiri njia ya kupitisha mkojo. Hivyo basi wanapendekeza wawe na mazoea ya kwenda haja dakika 15 kabla ya kushiriki tendo la ndoa.

Utafiti uliochapishwa katika jarida la matibabu la ustawi wa familia(2002) unasema kuwa wanawake wenye afya ambao huenda haja dakika 15 kabla ya kujamiiana huenda wakajiepusha na hatari ya kupata maambukizi wakilinganishwa na wenzao ambao hawafanyi hivyo.

Mapendekezo makuu:

 • Osha sehemu za siri kila siku kwa kutumia maji.
 • Piga mswaki.
 • Valia nguo za ndani safi, zilizotengenezwa kutokana na pamba ni bora zaidi.
 • Muone daktari angalau mara moja kwa mwaka ufanyiwe uchunguzi wa kimatibabu.
 • Kuwa na mazoea ya kujichunguza endapo utaona mabadiliko yoyote katika sehemu za siri muone dakatari.
 • Tumia kondomu wakati wa tendo la ndoa.
 • Inapendekezwa usiwe na mazoea ya kunyoa nywele zote zinaoota katika sehemu za siri, kwasababu zinatumika kama kinga, bora kupunguza kidogo.

Chanzo: Thamara Martínez Farinós, mwanasaikolojia na mtaalamu ya masuala ya ngono katika Taasisi ya Espill.

(Visited 19 times, 1 visits today)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here