Home Makala Fahamu kwa nini wazee katika eneo la Kilifi huko Kenya wanahofia maisha...

Fahamu kwa nini wazee katika eneo la Kilifi huko Kenya wanahofia maisha yao?

Visa vya wazee kuuwawa katika jimbo la Kilifi, pwani ya Kenya si jambo jipya. Aidha katika kipindi cha miaka miwili pekee, zaidi ya wazee 150 wameuwawa kwa madai ya kuwa wachawi, ama washirikina.

Lakini ni nini haswa chanzo cha mauaji hayo?

Mwanahabari wa BBC Roncliffe Odit amezuru kijiji cha Buni Kisimani, jimbo la Kilifi, ili kutupatia taswira halisi ya mauaji hayo.

Makaburi ndio yanayokukaribisha katika kijiji cha Buni Kisimani, jimbo la Kilifi nchini Kenya. Eneo hili limejaa vijana wanaoendesha boda boda; lakini wazee wenye mvi, au nywele nyeupe hawaonekani.

Na katika Eneo hili la jamii ya Mijikenda, kila unapotaja jina mzee, kiwewe kinawaingia. Kwanza nimekutana na Bi Chirindo Chisubi, mwenye umri wa miaka 63, aliyeachwa mjane baada ya mumewe kuuwawa kwa kisingizio cha kuwa mchawi.

Mjane huyu anasema mumewe aliuwawa na kakake, na japo alidhaniwa kuwa mchawi, yeye anaamini sababu kubwa ni kipande cha ardhi ambacho walirithishwa na wazazi wao.

‘Niliulizwa hata na polisi, je mumeo ni mchawi? Nikawaambia mimi tangu anioe sijawahi kuona chochote… maana wana shamba la baba yao, alipokufa sasa ilikuwa wamuite mtu wa ukaguzi ili wagawane.’

Ardhi imetajwa kuwa chanzo cha mauaji hayo

Mita chache tu kutoka hapa ni kaburi la babake Mwakoyo Dzayo aliyeuwawa mwaka huu. Aidha Mwakoyo Dzayo pia anakiri kwamba babake aliuwawa kwa kisingizio cha kuwa mshirikina, madai ambayo yeye anakana.

‘Sijamuona hata siku moja, kwa sababu mchawi ni yule ambaye katika kizazi chake unaweza kupata mtoto mmoja ambaye ni mlemavu, au hata upate kitu ambacho kitaashiria uchawi, lakini kwa babangu sijawahi kuona chochote kama hicho.’

Sasa ukweli ni nini kuhusu mauaji haya? Kamanda wa Polisi Jimbo dogo la Rabai Fred Abuga anasema tamaa ya kuwa na mali ya haraka ndio inayochochea mauaji haya.

Kamanda wa Polisi Jimbo dogo la Rabai Fred Abuga anasema tamaa ya kuwa na mali ya haraka ndio inayochochea mauaji haya.

‘Chanzo haswa cha haya maneno kulingana na uchunguzi wetu ni mambo ya mashamba. Unapata kwamba wazee wengi wakongwe ndio bado wenye vyeti vya mashamba. Sasa vijana ambao wamekuwa hawajahusishwa kikamili, hawana mashamba, na hawana njiia ya kukithi mahitaji yao>’

Lakini sasa nini kinachopaswa kufanywa ili kujaribu kupunguza mauaji haya?

Khamisi Mwaguzo ni mratibu wa shirika la Kenya Muslim Youth Alliance ambalo linajaribu kutatua kitendawili hiki.

Mwaguzo anasema lazima kila mtu ahusishwe kikamilifu katika kutafuta suluhu.

‘Wakristo, Waislamu, na hata Wazee wa Kaya (dini ya kitamaduni) lazima waje pamoja na kuhubiri amani, na kuieleza jamii kwamba hakuna uchawi. Pia lazima vijana waelimishwe jinsi ya kujitafutia wenyewe mali, badala ya kutegemea mashamba ya wazee wao.’

Lakini wakati familia zilizopoteza wapendwa wao zikiendelea kuomboleza, walio hai kwa sasa wanaishi kwa uoga wa kufumaniwa na kuuwawa kwa kisingizio cha uchawi.

Wazee wanauawa Kilifi kwa madai ya kuwa wachawi

Daniel Mwawara Garero ni mwenyekiti wa wazee wa Kaya hapa Rabai.

‘Wakati tukiendelea na haya mazungumzo kuna mzee wetu wa Kaya Chonyi yuko Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Kilifi. Na hata kwa boma letu, kuna mzee amechinjwa juzi tu, kwa hiyo bado mauaji yako na sote tunaishi na uoga.’

(Visited 1 times, 1 visits today)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here